NCCR-Mageuzi MKUTANO NA WANAHABARI TAREHE 14 MEI 2025, JIJINI DAR ES SALAAM

Ndugu zetu Wanahabari;
Tunawashukuru kwa kufika.
Tumewaalika hapa ilituweze kuwafikia watanzania wenzetu kuhusu utaratibu wetu na msimamo wetu kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao, ambapo kampeni zake zitaanza mwezi Agosti mwaka huu, 2025.
Ndugu zetu Wanahabari,
Kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao, sisi NCCR-Mageuzi kupitia kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika Jijini Dodoma tarehe 30 Machi, 2025, chama kimejipanga kushiriki kikamilifu kwa kusimamisha wagombea katika nafasi zote: Udiwani, Uwakilishi katika Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Ubunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania JMT), Urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na Urais wa JMT.
Tunaiomba Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi kuendelea kutoa Ushirikiano katika kufanya zoezi hilo, la Uchaguzi, kuwa la Amani, Huru na Haki, kama Rais alivyokwisha kutamka. Tunaamini kwa kushirikiana, elimu ya Uraia itatolewa kwa wapiga kura, malalamiko yote ya hilo zoezi yatashughulikiwa kwa wakati muafaka na kwa haki.
Tunawaomba wapiga kura kutumia haki yao ya Kikatiba kushiriki kikamilifu, hasa katika kupiga kura. Takwimu zinatuonesha ya kwamba, tangu mwaka 2000, katika uchaguzi mkuu ushiriki unakuwa chini. Hii inachangiwa sana na watanzania kukata tamaa.
Ndugu zetu Wanahabari,
Shughuli ni Watu! Hivyo tunawaomba watanzania wote wanaoamini kwamba kwa kujali UTU wetu, haki msingi za kila mtanzania zitapatikana, wajiunge na Chama chetu. Na pia tunaomba mwanachama yeyote anayetamani kugombea nafasi husika, kujitathmini kwa kuzingatia sifa zifuatazo za kiongozi:-
- Mwenye maadili ya Kitanzania;
- Mwenye kusimamia maslahi ya wengi dhidi ya wachache, ndani na nje ya nchi; na
- Mwenye kusimamia na kutetea Katiba ya JMT;
Hapa tunasisitiza, mwanachama mwenye uwezo wa:
- Kushirikisha wananchi katika mipango ya maendeleo ya umma; na
- Kufanya maamuzi magumu kwa maslahi ya wengi.
Ndugu zetu Wanahabari,
Tunapenda kuwataarifu watanzania wenzetu kwamba zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea katika nafasi mbalimbali zilizoainishwa, zitatolewa na katika ofisi ya Katibu Mkuu hivi karibuni na tutautaarifu umma juu ya hilo.
Tunawaomba Watanzania wote wenye kukubaliana na Itikadi yetu ya UTU na misingi yake na ajenda yetu ya UZAWA ambapo sisi tunaamini kuwa uchumi wa Taifa letu ukiwa mikononi mwa Wazawa, basi vijana wetu watapata ajira lakini pia Wazawa kwa uzalendo wao watalipakodi zinazopaswa kulipwa kwa wakati ili kujiunga na chama chetu, na pia wanachama wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi ilizoainishwa.
Asanteni kwa kunisikiliza;
Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.
Kwa Pamoja Tutashinda
………………………
Evaline Wilbard Munisi
KATIBU MKUU