Pamoja Tutashinda

TAMKO LA CHAMA CHA NCCR-MAGEUZI KUHUSU MAKINIKIA

 • Posted by admin
 • On June 19, 2017

TAMKO LA CHAMA CHA NCCR – MAGEUZI KUHUSU RIPOTI YA PILI YA MCHANGA WA MADINI YA DHAHABU (MAKINIKIA).

 

Chama cha NCCR-Mageuzi kilipoasisiwa Mwaka 1992 msingi Mkuu wa sera yake ilikuwa ni UZAWA. Chama cha NCCR-Mageuzi kinaamini katika Utajiri Mkubwa wa Mali asili ambazo Tanzania tumejaliwa, na Madini ni sehemu moja tuu ya maliasili tulizonazo. Baadhi ya maliasili tulizonazo ni pamoja na; Mbuga za Wanyama, Makumbusho ya kale, Milima, Misitu, Tamaduni zetu, Bandari asili (Natural Harbor), Bahari, Maziwa, Mito na Ardhi yenye rutuba n.k.

 

NCCR-Mageuzi tuliona wazi kuwa Sera za Chama cha Mapinduzi zilikuwa hazimnufaishi Mtanzania mzawa ndio maana tulikuja na sera ya UZAWA ambayo kwa umakini na uchungu mkubwa ikazaa Itikadi sera za UTU, kwamba rasilimali zote tulizonazo ni za Mtanzania na ni muhimu zikamnufaisha Mtanzania. NCCR-Mageuzi tulipingwa wazi wazi na Chama cha Mapinduzi na kuja na propaganda kuwa tulikuwa waleta fujo na uchochezi katika Sera ya Ubaguzi. Lakini msingi wa sera yetu ilikuwa ni rasilimali ziwanufaishe kwanza Watanzania Wazawa ambao ni watoto wa wakulima na wafanyakazi ambao ni masikini sana.

Suala la kuibiwa rasilimali zetu hasa za madini, NCCR-Mageuzi tulianza kulipigia kelele siku nyingi sana mtakumbuka katika Bungeni la mwaka 1995-2000 Chama cha NCCR-Mageuzi ndicho chama kilichokuwa na wabunge wengi kwa vyama pinzani, kikiwa na hazina kubwa ya wasomi waliokuwa na Uchungu na Nchi hii, na hata sheria zlizopitishwa mwaka 1997 wabunge wa NCCR-Mageuzi ambao wengi wao walikuwa ni wanasheria  walizipinga sana kuwa sheria hizo zilikuwa ni kandamizi, hazikuwa na maslahi kwa wa Tanzania. Ni watendaji wa serikali na wabunge wa CCM walitupinga na kulazimisha kupelekea kutengeneza sheria mbovu na kuingia mikataba mibovu mwaka 1998 na ndio zao la matokeo ya leo kwani haya makampuni ya Mchanga mwaka 1998 ndipo yalipoanza kazi za uchimbaji wa madini.

 

SHERIA MBOVU NA USIRI WA MIKATABA

NCCR – Magauzi tangu Mwaka 1992 na hata kwenye Bunge la Mwaka 1995-2000 tulizungumzia sana suala la sheria mbovu kuanzia Sheria mama yaani Katiba. Ikumbukwe NCCR-Mageuzi ndio waasisi wa suala la KATIBA YA WANANCHI na hata asili ya NCCR ilikuwa ni Kamati Ya Kuratibu Mabadiliko Ya Katiba ambapo tungelipata dhamana ya kuongoza nchi tungesimamia upatikanaji wa Katiba inayotokana na wananchi yenye vifungu vya kulinda rasilimali zetu hasa maliasili , lakini Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilipinga kwa muda mrefu ikitetea kuwa ina Katiba nzuri na sheria nzuri lakini leo hii Kamati zilizoundwa na Rais zinawaumbua kuwa tuna sheria Mbovu ambazo zilipitishwa na Bunge lenye wabunge wengi wa Chama cha Mapinduzi.

Suala lingine lilikuwa ni Usiri Wa Mikataba, miaka yote NCCR – Mageuzi tumekuwa tukipigania  suala la usiri wa mikataba na hili sio kwamba  linafanywa kwa bahati mbaya bali ni suala linalofanywa kwa makusudi na Watanzania wenzetu ambao hawana uchungu na nchi hii, likapata Baraka za serikali ya CCM kwa makusudi maalumu. Upinzani unapambana katika mazingira magumu yenye kebehi, kuonewa, kuchekwa wakati wa vipindi vya bunge, na hata kuna waziri alisimama mbele ya Bunge na kusema mikataba ya siri “alitumia neno la kiingereza” ni (best practice) Kwa hiyo inashangaza na kuuma sana leo hii eti Serikali ya CCM ndio inasikitika na kulia kuwa tunaibiwa.

Chimbuko

na Sababu kuu zilizo sababisha ufisadi wa kupindukia na  nchi yetu kuchelewa kupiga hatua ya maendeleo na kubaki katika umasikini ulio kithili wakati inazo rasilimali za kutosha ni pamoja na;

 1. Kushindwa kupatikana katiba ambayo ni zao la wananchi wenyewe, ambayo ingewapa mamlaka ya kuwadhibiti watawala.

 

 1. Uchumi kutumikie siasa badala ya siasa kutumikia uchumi na hili nizo la kutokuwa na mipango shilikishi kuanzia ngazi ya chini (yaani bottom up approach) sambamba na kupuuza ushauri wa kitaalamu katika sera mipango na utekelezaji. kwa makusudi maalum.

 

 1. Ukosefu wa Uongozi wenye Uzalendo, Uadilifu na Utawala bora ambao umepelekea Uzembe, Kutowajibika, Kukithiri kwa ufisadi na Ubadhirifu wa mali za umma.

 

 

CCM IJIULIZE, IJIPIME NA IWAOMBE RADHI  WATANZANIA

 1. Kamati zote mbili zilizoundwa na Rais wa jamuhuri ya muugano wa Tanzania zimethibitisha pasipo na shaka kuwa Watanzania tunaibiwa tena kwa kiwango kikubwa sana. Lakini sio kamati hii tu ndio imesema, kuna Kamati Ya Bomani ya Mwaka 2007 ilikuwa na Maoni na mapendekezo mengi lakini hayakufanyiwa kazi na chama kilichokuwa kinendelea kupewa dhamana na wananchi pamoja na wabunge wengi bugeni – CCM.

 

 1. Kukiri Kosa ni Uumgwana na Hatua ya Kuanza Kupimwa Tena Kuaminika. CCM ijitokeze hadharani na kuwaomba radhi Watanzania kuwa hawakuwatendea haki pia wajitathmini kama kuna haja ya watanzania kuendelea kuwaamini kuwapa ridhaa ya kuongoza Nchi maana haya yaliyotokea ni eneo dogo la MCHANGA WA MADINI (MAKINIKIA). NCCR – Mageuzi tunaamini kuwa baado kuna madudu mengi zaidi na hatujui mikataba iliyosainiwa imetuumiza kwa kiasi gani.

 

 1. Hatua kali za kisheria zichukuliwa dhidi ya yeyeyote aliyeshiriki katika kuangamiza uchumi wa taifa. (hekima, busara na sheria viwe ndo mhimili mkuu katika kufikia hatima ya jambo hili kubwa badala ya siasa – Natural justice)

 

USHAURI:

Pamoja na kuunga Mkono jitihada za kuokoa rasilimali zetu tunashauri kuwa:

 1. Kwanza NCCR-Mageuzi tumefarijika sana kuona yale yote tuliyokuwa tunayapigania kwa Miaka mingi yanaendelea kwa kasi kudhihirika wazi wazi, kwani mawazo yetu yalikuwa ni Chanya na leo hii ukweli unaendelea kudhihirishwa na Kamati zilizoundwa na wasomi

 

 1. Serikali iyafanyie kazi kwa Umakini, Hekima Na Busara kubwa mapendekezo yaliyotolewa na kamati zote mbili zilizoundwa kuchunguza suala la Makinikia na athari tulizozipata kiuchumi.

 

 1. Hatua kali za kisheria zichukuliwa dhidi ya yeyeyote aliyeshiriki katika kuangamiza uchumi wa taifa. (hekima, busara na sheria viwe ndo mhimili mkuu katika kufikia hatima ya jambo hili kubwa badala ya siasa – Natural justice)

 

 1. Kuwepo na kamati maalum ya wataalamu wa kisheria itakayoshauri hatua za kuchukua kisheria bila kuligharimu Taifa, maana tatizo la kwanza lililoonekana ni Ubovu Wa Sheria Zetu ambazo zilitoa mianya ya kuingiwa kwa Mikataba Mibovu. Pili ni Ubovu Wa Mikataba iliyosainiwa na watu waliopewa dhamana na serikali ya kusaini mikataba kwa niaba ya Watanzania.

 

 1. Tunaunga mkono Ripoti zote mbili kupelekwa Bungeni zikajadiliwe na wawakilishi wa wananchi.

 

 

 1. Mbali ya kuunga mkono suala la kupitiwa upya sheria zote zinazohusu masuala ya madini, pia ni wakati muafaka wa wataalamu wazalendo kuipitia tena Sheria Mama hasa Katiba Inayopendekezwa kabla ya Kupigiwa Kura Ya Maoni ili kuangalia kuwa katika Katiba inayopendekezwa ambayo ilipitishwa na wabunge wa CCM mambo haya yamezingatiwa kwa sababu kama Rais anataka tumuunge mkono katika Vita Vya Uchumi basi lazima kuwe na Katiba inayosaidia kutunga sheria zenye maslahi kwa Watanzania. Sisi NCCR – Mageuzi bado tunaona kuna maoni mengi yaliyokuwa kwenye Tume Ya Warioba yana umuhimu mkubwa wa kuendelea kuwemo

 

 1. Suala la Maadili na Miiko ya Uongozi ambavyo vilikuwa katiba Rasimu Ya Tume Ya Warioba ni muhimu vikapitiwa upya na kuongezwa kwenye Katiba inayopendekezwa kwa sababu baadhi ya watu ambao ni wanasheria ambao walionekana ni washauri wakubwa katika Bunge la Katiba, leo hii ndio wanatuhumiwa kuwa waliisababisha Nchi kuwa na sheria Mbovu, Mikataba Mibovu. Ni vema kama nchi yenye dira thabiti kujilidhisha kama hapakuwa na ushawishi wa kimasilahi.

 

 

 1. Kamati itakayoundwa kupitia Sheria za Madini na Kamati itakayoundwa kupitia Mikataba yote mikubwa tunaomba iangalie katika Hansard za Bunge kuanzia mwaka 1995 kuangalia maoni mazuri yaliyotolewa na wabunge na hasa wakati wa mjadala wa sheria ya madini miaka ya 1997 Kuona maoni ya kambi ya upinzani. Pia hizo kamati ziangalie maoni na mapendekezo ya CAG maana amekuwa anatoa maoni mengi lakini yamekuwa hayafanyiwi kazi.

 

 

 1. Kuna haja ya kuangalia na Maeneo mengine yanayoweza kuchangia Uchumi mkubwa, mfano; Sekta ya Utalii ambapo kuna mbuga na Vivutio vikubwa sana hapa inchini, haja ya kuunda kamati maalum ya wataalamu ili kulishauri Taifa hatua za kufanya maana kumekuwa na hisia mbaya ya sakata ya Vitalu.

 

 1. Kujenga uchumi shilikishi unaolenga kupunguza umasikini na Kujenga ushirikiano wa karibu baina ya serikali na sekta binafsi na mifumo bora ya taasisi za serkali kuaminiana.

 

 1. Kuitishwa Bunge Maalum La Katiba. Kwa mtiririko wa mambo yanayoendelea kuhusu Hatima Ya Taifa Letu, Rais, kwa ujasiri huu huu aone umuhimu wa kuchukua uamuzi wa kuita tena Bunge Maalum La Katiba kupitia tena vifungu vyote vya Katiba Inayopendekezwa ili kuhakikisha kuwa vina manufaa kwa Watanzania bila ya kujali itikadi za Vyama. Maana yote yanayotokea sio kwamba yanatokea kwa bahati mbaya bali ni kutokana na Msingi Mbovu Wa Katiba Ya Nchi. Lazima tukubaliane kuwa katiba inayopendekezwa ilipitishwa kwa Ushabiki Mkubwa wa kisiasa kwa hiyo kuna haja ya kukutana na kufanya maridhiano ya Kitaifa

 

HITIMISHO:

NCCR –Mageuzi  Kwa Msingi Wetu Mkuu wa Kuamini katika Demokrasia ya Kijamii, tutabariki, kupongeza, kuunga mkono  na kuheshimu mchango wa kiongozi yoyote wenye maslahi na ustawi  wa Taifa letu.  Tutaendelea kuelimisha, Kutetea, Kutoa maoni, na Michango ya kiutafiti katika kujenga mama yetu Tanzania. Pia tutaendelea kukosoa na hata kulaani vitendo hovu inapobidi.

NCCR – Mageuzi itaendeleza juhudi zote za kutetea rasilimali zote zitumike kumnufaisha Mtanzania Mzawa na hii ndio Sera Ya Uzawa, Sera iliyo asisiwa na Chama Chetu Cha NCCR – Mageuzi ambayo tume kuwa tunaipigania kwa thamani kuu  miaka yote kuwa ndio sera itakayomkomboa Mtanzania Masikini pamoja na elimu bora na upatikanaji wa katiba bora inayotokana na Mzawa

Hivi sasa NCCR-Mageuzi inasimamia ITIKADI YA UTU kwamba UTU wa Binadamu hasa Mtanzania una thamani kubwa sana kwa hiyo Katiba na sheria zote, Mipango na Mikakati yote ni lazima ifanyike kuinua UTU WA MTANZANIA.

 

 

JUJU MARTIN DANDA

KATUBU MKUU

(NCCR – MAGEUZI).

0 Comments

Leave Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *